Ayatullah Seyyed Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya
Kiislamu ameyasema hayo leo alasiri mjini Tehran alipokutana na kufanya
mazungumzo na Ramadhan Abdullah, Kiongozi wa Harakati ya Jihad Islami ya
Palestina. Akitoa tathmini jumla kuhusu hali ya hivi sasa katika eneo
amesisitiza kuwa: "Vita vipana vinaendelea sasa katika eneo. Vita hivi
ni muendelezo wa vita vya miaka 37 iliyopita ambavyo vilianzisha dhidi
ya Iran."
Kiongozi Muadhamu amesisitiza kuwa, msimamo wa Iran kuhusu Palestina si
msimamo wa kipindi fulani tu na kuongeza kuwa: "Kabla ya ushindi wa
Mapinduzi ya Kiislamu na katika zama za mapambano, msimamo wa kuunga
mkono Palestina na kukabiliana na utawala wa Kizayuni ulikuwa msimamo wa
mara kwa mara wa Imam Khomeini MA na baada ya ushindi wa Mapinduzi ya
Kiislamu vile vile, kuunga mkono watu wa Palestina kulikuwa moja kati ya
hatua za awali za Iran. Kwa hivyo kuunga mkono malengo matukufu ya
Wapalestina, ni jambo ambalo liko katika dhati ya Jamhuri ya Kiislamu ya
Iran."
Ayatullah Khamenei ameashiria mashinikizo mbali mbali na mapana ya
kisiasa, kipropaganda ,kiuchumi na hata ya kijeshi ili kupigisha magoti
Mapinduzi ya Kiislamu au kuufanya mfumo wa Kiislamu uachane na misimamo
yake. Ameongeza kuwa, kile ambacho kinajiri leo katika eneo ni
muendelezo wa makabiliano ya Marekani na Mfumo wa Kiislamu wa Iran.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema lengo kuu la vita
vipana vya sasa vya mrengo wa Magharibi ukiongozwa na Marekani dhidi ya
mrengo wa Kiislamu ni kulidhibiti eneo la Magharibi mwa Asia. Amesema
matukio ya eneo hili yanapaswa kutathminiwa kwa mtazamo huu; na kwa
msingi huo, masuala ya Syria, Iraq, Lebanon, na Hizbullah ni kati ya
makabiliano haya.
Ayatullah Khamenei amesisitiza kuwa, katika hali kama hii, 'kutetea Palestina ni nembo ya kutetea Uislamu"
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ameongeza kuwa, mrengo wa madola ya
kibeberu na kiistikbari yametekeleza jitihada kubwa kwa ajili ya
kuarifisha makabiliano ya sasa katika eneo kuwa eti ni 'vita baina ya
Shia na Suni.
Ayatullah Khamenei amebaini kuwa, "nchini Syria serikali si ya Kishia ,
lakini Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaunga mkono serikali ya Syria. Hii
ni kwa sababu watu wanaokabiliana na Syria ni maadui wa Uislamu na
wanahudumia maslahi ya Marekani na utawala wa Kizayuni."
Ayatullah Khamenei aidha ameashiria matamshi ya Katibu Mkuu wa Jihad
Islami kuhusu baadhi ya njama za kuishinikiza harakati ya Hizbullah ya
Lebanon na kusema: "Hizbullah ya Lebanon ina nguvu zaidi na haiwezi
kuathiriwa na hatua dhidi yake. Leo bila shaka utawala wa Kizayuni
unaiogopa Hizbullah zaidi."
3493905