IQNA

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

Adui anaendesha vita laini na vya siri dhidi ya Iran

18:40 - October 02, 2016
Habari ID: 3470593
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuhimiza kumbukumbu ya mashahidi ni moja ya nukta muhimu katika kukabiliana na njama za adui na kulinda mapambano katika jamii.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Seyyed Ali Khamenei aliyasema hayo katika kikao na wanachama wa Idara ya Kongamano la Mashahidi wa Mikoa ya Kohgiluyeh na Boyer-Ahmad na Khorassan Kaskazini. Kikao hicho kilifanyika Septemba 26 na maelezo yake yamechapishwa leo Jumapili.

Katika kikao hicho, Kiongozi Muadhamu alisema lengo la vita laini na vya siri vya adui ni kuwaweka mbali wananchi na medani ya jihadi na mapambano na kuwafanya wapuuze malengo matukufu sambamba na kuyateka mazingira ya kifikra na kiroho nchini.

Ayatullah Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameendelea kusema kuwa, 'Taifa la Iran kwa muqawama, mapambano na kusimama kidete,  limeweza kusambaratisha malengo mengi ya madola makubwa duniani".

Ayatullah Khamenei ameongeza kuwa, madola ya kibeberu yanatumia vyombo mbali mbali kueneza propaganda pana sambamba na mashinikizo ya kisiasa, kiuchumi na kiusalama ili kuwafanya wananchi wa Iran wapoteze matumaini na hatimaye waondoke katika medani.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuhusu udharura wa kubainisha kuhusu vita vya kulazimishwa (vya Saddam dhidi ya Iran) na kuongeza kuwa: "Kujihami kutakatifu kulikuwa ni vita vya kimataifa dhidi ya Uislamu, dhidi ya utawala wa Kiislamu na dhidi ya Imam Khomeini MA." Amesema Saddam wa chama cha Baath ambaye alikuwa dhalili na asiye na akili alipata uungaji mkono wa pande zote na hivyo vijana wa leo wanapaswa kuwafahamu kikamilifu wale ambao walisimama kidete katika kuiokoa nchi kutokana na shari kama hii.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislam amesema Mashahidi  ni 'Ngome ya Akhlaqi za Kiislamu' na ni 'Kigezo kwa ajili ya kizazi cha vijana' na kuongeza kuwa wasanii wanapaswa kuwaonyesha vijana taswira iliyojaa nuru ya mashahidi kwa kutumia mbinu mbali mbali hasa uandishi wa vitabu vifupi visivyotia chumvi na vinavyoonyesha uhalisia wa maisha yao.

3534656

captcha