IQNA

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

Marekani inapinga Iran iliyostawi na inayofuata misingi ya Kiislamu

10:14 - October 20, 2016
Habari ID: 3470621
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, maudhui ya utandawazi na maagizo ya Wamarekani na watu wa Ulaya wanaoitaka Iran kujiunga na eti "familia ya kimataifa" ni mfano wa wazi wa kuzalishwa tena utamaduni wa kuwa tegemezi.

Ayatullah Ali Khamenei ameyasema hayo Jumatano mjini Tehran alipohutubia mkutano wa wasomi na watu wenye vipawa bora na vya juu zaidi vya kielimu hapa nchini na kuongeza kuwa, upinzani dhidi ya kile Wamagharibi wanachokiita jamii ya kimataifa si upinzani dhidi ya kuwa na mawasiliano ya kigeni bali maana yake ni kusimama kidete dhidi ya utamaduni wa kutwishwa na madola makubwa katika masuala ya uchumi, siasa na usalama.

Ayatullah Khamenei ameashiria uadui wa madola ya kishetani dhidi ya harakati yoyote ya upinzani na kuongeza kuwa: Matamshi yaliyotolewa na kiongozi mmoja wa Marekani kuwa Iran inauunga mkono muqama na mapambano na kudumishwa vikwazo dhidi ya Iran vinaakisi uhakika wa kuwa na mtazamo mbaya kuhusu Marekani.

Vilevile ameashiria taarifa iliyotolewa hivi karibuni na Umoja wa Ulaya ambayo imezungumzia suhula na uwezo mkubwa wa Iran na kuongeza kuwa, matamshi yanayohusu maendeleo,rasilimali watuna maliasili ya Iran si porojo, bali ni uhakika ambao hata Wamagharibi wanaukubali.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa, hapana shaka kuwa Wamarekani wanapiga vita Iran yenye uwezo na maendeleo kama hayo na serikali yenye misingi ya Kiislamu, na kujulikana na kuchambuliwa vyema suala hilo baina ya vijana wenye vipawa vya juu kutawasaidia katika kutekeleza vyema majukumu yao ya kihistoria.

Ayatullah Khamenei amegusia pia masaibu na matatizo ya dunia ya sasa na mkwamo wa fikra za kimaada na kusema: Ulimwengu unahitaji fikra mpya katika masuala ya kibinadamu na kimataifa. Amesema kuwa, ushindani wa uchaguzi wa Marekani na masuala yanayozungumziwa katika kampeni za wagombea wawili wa kiti cha rais wa nchi hiyo ni mfano wa wazi wa matokeo ya kutokuwepo masuala ya kiroho na imani kati ya wenye madaraka na nguvu.

Ayatullah Khamenei amesema kuwa, katika wiki kadhaa zijazo mmoja kati ya wagombea hao wawili katika uchaguzi wa Marekani atakuwa rais wa nchi yenye nguvu na utajiri mkubwa zaidi,silaha nyingi zaidi za nyuklia na vyombo vikubwa zaidi vya habari duniani.

Ameeleza sababu ya udharura wa viongozi kutilia maanani na kulipa mazingatio maalumu suala la wasomikuwa ni malengo makubwa yanayokusudiwa na utawala wa Kiislamu. Ameongeza kuwa: Jamhuri ya Kiislamu inapaswa kuwa nchi iliyoendelea, yenye nguvu, sharifu, yenye fikra mpya, yenye izza na hadhi kubwa, uliyojaa masuala ya kimaanawi na kiroho, imani na inayopeperusha bendera ya ustaarabu mpya wa Kiislamu.

3539102

captcha