Ayatullah Sayyid Ali Khamenei aliyasema hayo jioni ya jana alipokutana
na Rais Nicolás Maduro wa Venezuela ambapo sanjari na kuashiria kufeli
kwa njama na siasa za Marekani katika eneo la magharibi mwa Asia,
amegusia suala la kushushwa bei ya mafuta kuwa ni nyenzo ya
kuzishinikiza nchi huru.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu
ameelezea utumiwaji wa silaha ya mafuta kwa ajili ya kuzitwisha matatizo
nchi zinazojitegemea na kusema, wakati wa nyuma pindi baadhi ya nchi za
Kiislamu zilipouwekea vikwazo vya mafuta utawala haramu wa Kizayuni,
Wamagharibi, walitumia siasa ya mafuta kueneza makelele yao na kwamba
kwa bahati mbaya nchi hizo hizo hii leo zimegeuka na kuwa waratibu
wakubwa wa siasa za Marekani kupitia silaha ya mafuta.
Kiongozi Muadhamu
ameashiria nafasi chanya ya Venezuela katika harakati dhidi ya
uistikbari katika eneo la Amerika ya Latini kuwa ishara ya nafasi ya juu
ya nchi hiyo sambamba na kumtaka rais wa taifa hilo atumie fursa ya
uenyekiti wake wa Harakati ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande
wowote NAM kufikia malengo yanayotarajiwa.
Ameongeza kuwa, Wamagharibi hawafurahishwi na harakati za jumuiya hiyo
lakini akasisitiza kuwa, nchi huru lazima zisimame kukabiliana na njama
hizo za Wamagharibi kwani kwa mwenendo huo kutaweza kufikiwa mustakbali
mwema.
Kwa upande wake Rais Nicolás Maduro wa Venezuela sanjari na
kupongeza muqawama wa taifa la Iran katika kukabiliana na adui Marekani
amesema, katika hali ambayo raia wa taifa hili wanaishi kwa usalama na
amani, akthari ya nchi nyingi za eneo na majirani zake wanaishi katika
vita, tofauti na udhaifu.
Ameashiria kupungua kwa bei ya mafuta katika
kipindi cha miaka miwili iliyopita na kuongeza kuwa, licha ya uingiliaji
wa ubeberu wa Marekani na uadui mkubwa dhidi ya Venezuela, lakini raia
wa nchi hiyo wamesimama kidete kukabiliana na vita vya kiuchumi na sasa
wanaepukana taratibu na mgogoro huo.
3539912