IQNA

Jeshi la Myanmar laua Waislamu 150 jimboni Rakhine

11:07 - November 17, 2016
Habari ID: 3470682
IQNA-Jeshi la Myanmar limeua Waislamu wasiopungua 150 wa jamii ya Rohingya katika jimbo la Rakhine.

Kwa mujibu wa Jumuiya ya Kitaifa ya Arakan ya Rohingya yenye makao yake London, Jumamosi wiki hii hadi sasa Waislamu wasiopungua 150 wa jamii ya Rohingya wameuliwa katika hujuma ambazo zimetekelezwa na jeshi huku serikali ya Myanmar ikijaribu kuzuia vyombo vya habari na makundi ya utoaji misaada yasifike katika eneo la maafa ili kuficha ukweli kuhusiana na mauaji hayo.

Serikali ya Myanmar imethibitisha kuuawa Waislamu wapatao 70 wa jamii ya Rohingya katika machafuko yaliyotokea siku chache zilizopita katika eneo la Rakhine.

Hatua kali za usalama zimechukuliwa kaskazini mwa eneo la Rakhine tangu tarehe 9 ya mwezi uliopita wa Oktoba, sambamba na kile kilichoelezwa kuwa shambulio dhidi ya askari wa mpakani ambapo askari polisi tisa waliuliwa.

Serikali ya Myanmar inadai kuwa eti Waislamu wa jamii ya Rohingya kuwa ndio waliofanya shambulio hilo huku ripoti rasmi zikieleza kwamba makumi ya watu wameuliwa na kutiwa nguvuni katika msako wa jeshi wa kuwatafuta wahusika wa mauaji hayo.

Wakaazi wa eneo la Rakhine na wanaharakati wa haki za binadamu wanaeleza kuwa katika mashambulio ya vikosi vya serikali jinai mbalimbali zinafanywa dhidi ya raia ikiwemo kuua watu bila ya sababu, ubakaji na kuchomamoto nyumba zao.

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa Waislamu wa kabila la Rohingya ni jamii ya wachache duniani inayodhulumiwa na kunyongeshwa zaidi. Serikali ya Myanmar inakataa kuwapa haki za uraia Waislamu ambao idadi yaoni zaidi ya watu milioni moja na laki tatu. Mabudhha wenye misimamo mikali Myanmar wanashirikiana na serikali katika kuwakandamiza, kuwatesa na kuwaua kiholela Waislamu.

Katika miaka ya karibuni, Waislamu wengi wa kabila la Rohingya nchini Myamnar wameuawa au kulazimika kuhama makazi yao na kuwa wakimbizi katika nchi za Thailand, Malaysia na Indonesia.

3546683

captcha