IQNA

Maelfu ya Waislamu wa Myanmar wakimbilia Bangladesh kuokoa maisha

20:30 - December 30, 2016
Habari ID: 3470768
IQNA: Makumi ya maelfu ya Waislamu wa kabila la Rohingya nchini Myanmar wamekimbilia katika nchi jirani ya Bangladesh ili kunusuru maisha yao.

Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Bangladesh imetangaza kuwa, Waislamu elfu 50 Warohingya kutoka wa jimbo la nchini Myanmar wamekimbilia nchini humo kujiokoa na vitendo vya ukandamizaji na utumiaji mabavu dhidi yao vinavyofanywa na jeshi la nchi hiyo pamoja na mabudha wenye misimamo mikali.

Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Bangladesh imemuita balozi wa Myanmar mjini Dhaka na kumuelezea wasiwasi iliyonao nchi hiyo kutokana na kuendelea vitendo vya ukandamizaji na utumiaji mabavu dhidi ya Waislamu wa jamii ya wachache ya Rohingya nchini Mynamar.

Myanmar yazuia meli ya misaada ya Malaysia

Wakati huo huo Utawala wa Myanmar unaendelea kuzuia msafara wa meli za Malaysia zinazosheheni misaada ya dharura kwa ajili ya Waislamu wa kabila la Rohingya huku uhusiano wa nchi mbili hizo ukiendelea kuzorota.

Msafara huo ulikuwa uondokeMalaysia kuelekea katika jimbo la Rakhine nchini Myanmar ambapo Waislamu wa kabila la Rohingya wanakabiliwa na hali ngumu ya maisha. Msafara huo ulipangiwa kuondoka Malaysia Januari 10 ukiwa na shehenaya tani 1,000 za mchele, dawa na mahitajio mengine ya dharura kwa ajili ya Waislamu wa Rohingya lakini wakuu wa Myanmar wamekataa kutoa idhini kwa meli hiyo.

Malaysia imekuwa ikiikosoa vikali serikali ya Myanmar kwa kuwakandamiza Waislamu katika jimbo la Rakhine ambapo katika miezi ya hivi karibuni maelfu ya Waislamu wanaripotiwa kuuawa kiholela huku wengine laki tatu wakilazimika kukimbia makazi na nyumba zao.

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa Waislamu wa kabila la Rohingya ni jamii ya wachache duniani inayodhulumiwa na kunyongeshwa zaidi. Serikali ya Myanmar inakataa kuwapa haki za uraia Waislamu hao ambao idadi yao ni zaidi ya watu milioni moja na laki tatu.

Katika miaka ya karibuni, Waislamu wengi wa kabila la Rohingya nchini Myamnar wameuawa au kulazimika kuhama makazi yao na kuwa wakimbizi katika nchi za Thailand, Malaysia na Indonesia kutokana na mashambulio ya Mabudha wenye misimamo ya kufurutu mpaka wanaoungwa mkono na serikali ya nchi hiyo.

3557802

captcha