IQNA

Watetezi wa Wapalestina

Ayatullah Khamenei: Kadhia za Gaza zimewadhihirishia walimwengu hakika nyingi zilizofichika

21:52 - November 19, 2023
Habari ID: 3477916
TEHRAN (IQNA)- Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema: kadhia za Gaza zimewadhihirishia walimwengu hakika nyingi zilizofichika, na moja wapo ya hakika hizo ni uungaji mkono wa viongozi wa nchi za Magharibi kwa ubaguzi wa rangi.
Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameyasema hayo leo mbele ya hadhara ya makamanda na maafisa wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia za Anga za Mbali cha Ashura baada ya kutembelea maonyesho ya mafanikio na uwezo wa kikosi cha Anga za Mbali cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC).
Ayatullah Khamenei ameutaja utawala wa Kizayuni kuwa ni dhihirisho la ubaguzi wa rangi na akaeleza kwamba, Wazayuni wanajiona wao ni wenye mbari bora na wanawaona wanadamu wengine wote kuwa ni wenye mbari duni na ni kwa sababu hiyo wameua maelfu kadhaa ya watoto bila nafsi zao kuhisi chochote.
 
Ayatullah Khamenei amesisitiza kuwa: wakati Rais wa Marekani, Kansela wa Ujerumani, Rais wa Ufaransa na Waziri Mkuu wa Uingereza pamoja na kujidai kwao kote wanauunga mkono na kuusaidia utawala huo wa kibaguzi, hiyo inamaanisha kwamba mabwana hao wanaunga mkono ubaguzi wa rangi, ambao ni jambo linalochukiwa zaidi duniani.

Amiri Jeshi Mkuu amebainisha kuwa: watu wa Ulaya na Marekani wanapaswa kuweka wazi msimamo wao juu ya suala hilo na kuonyesha kwamba hawaungi mkono ubaguzi wa rangi.

Ayatullah Khamenei aidha ameashiria kushindwa kijeshi na kioparesheni utawala wa Kizayuni na akasema: kushindwa utawala wa Kizayuni huko Gaza ni ukweli halisi; na kusonga mbele na kuingia katika hospitali au makazi ya watu si ushindi, kwa sababu ushindi maana yake ni kuushinda upande wa pili (wa mapigano) ambapo hadi sasa utawala wa Kizayuni haujaweza kuupata na hautaweza kuupata pia katika siku zijazo.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa, wigo huo wa kushindwa na akutoweza ni mpana zaidi na haukomei kwa utawala wa Kizayuni; na akafafanua kwamba: kutoweza na kushindwa huko kunamaanisha kushindwa Marekani na nchi za Magharibi pia, na hivi sasa ulimwengu mzima umedhihirikiwa na ukweli kwamba utawala wenye nyenzo na zana chungu nzima na za kisasa kabisa za kijeshi haujaweza kumshinda mpinzani wake ambaye hana nyenzo na zana hizo.

Katika hotuba yake hiyo, Ayatullah Khamenei vile vile amezungumzia wajibu na utendaji wa serikali za nchi za Waislamu na akasema: baadhi ya serikali za mataifa ya Waislamuu zimeonekana kulaani jinai za utawala wa Kizayuni katika hadhara mbalimbali, na baadhi yao hazijalaani hadi sasa, lakini hilo tu halikubaliki; hatua kuu na ya msingi ni kukatwa mshipa muhimu na wa mtiririko wa utawala wa Kizayuni kwa serikali za mataifa ya Waislamu kuzuia nishati na bidhaa zisiufikie utawala huo.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: watu wa mataifa inapasa waendeleze mikusanyiko na maandamano yao na kutoruhusu dhulma wanayofanyiwa wananchi wa Palestina ikasahaulika.

 
Habari zinazohusiana
captcha